Ujumbe wa Rais Dkt. Samia Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu zake za Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari akieleza kufurahishwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini.

Katika ujumbe wake uliochapishwa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia alieleza kuwa kupanda kwa Tanzania katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari duniani ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na wadau wote katika sekta hiyo muhimu.

“Kheri ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Ninafarijika kuona tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza, ambapo mwaka 2025 tumepanda zaidi katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Haya ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na kila mdau kwenye sekta hii muhimu,” amesema Rais Samia.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Rais Samia alitoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutumia weledi katika utendaji wao ili kuchangia katika kudumisha amani, utulivu, na umoja wa kitaifa. Amesisitiza kuwa vyombo vya habari ni washiriki muhimu katika shughuli za Serikali na kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.

“Ninaendelea kuvisihi vyombo vya habari kutumia weledi katika kazi zenu ili kuendelea kujenga na kuimarisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa, hasa kipindi hiki tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Ninyi ni wadau na washiriki muhimu si tu kwa shughuli za Serikali, bali pia kwa uhai wa Taifa letu,” aliongeza Rais Samia.