Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski, amerejea uwanjani baada ya kupona majeraha ya msuli wa paja (semitendinosus) aliyoyapata Aprili 19, 2025 katika mchezo wao dhidi ya Celta Vigo.
Majeruhi hayo yalimuweka Lewandowski nje ya uwanja kwa takriban wiki tatu, akikosa fainali ya Copa del Rey dhidi ya Real Madrid na mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan, iliyomalizika kwa sare ya 3-3 .
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amethibitisha kuwa Lewandowski amepona na ni sehemu ya kikosi kilichosafiri kwenda Milan kwa ajili ya mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan, lakini alitarajiwa kuanza mechi hiyo akiwa benchi.
Uamuzi huo umelenga kumlinda mchezaji huyo kutokana na hatari ya kurejea tena kwenye majeraha, hasa ikizingatiwa umuhimu wa mechi hiyo na ratiba ngumu inayofuata, ikiwa ni pamoja na El Clásico dhidi ya Real Madrid siku ya Jumapili, Mei 11, 2025.
Kwa msimu huu, Lewandowski amekuwa na mchango mkubwa kwa Barcelona, akifunga mabao 40 katika mechi 48 kabla ya kuumia.
Kurejea kwake kumeongeza matumaini ya Barcelona kufuzu kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka kumi, huku timu hiyo ikiongoza LaLiga na kutwaa taji la Copa del Rey.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.