Rais wa Namibia kufanya ziara ya Siku mbili nchini Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt.Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kufanya
Ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Tanzania kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025 kwa
mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa
Rais wa Jamhuri ya Namibia tarehe 21 Machi 2025 na inalenga kukuza ushirikiano
wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwemo katika nyanja za biashara, uwekezaji na elimu,

Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu wa kidugu na kidiplomasia,
hivyo ziara hii itafungua fursa mpya za ushirikiano zitakazowawezesha wananchi wa nchi
zote mbili kunufaika kiuchumi

Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais
Dkt. Samia ambapo viongozi hao wawili wanatarajia kuwa na mazungumzo ya uwili na
kisha kuongoza mazungumzo rasmi baina ya nchi hizo mbili na baadae kuzungumza na
waandishi wa habari.

Aidha, akiwa nchini Tanzania, Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah atatembelea Kituo cha Urithi wa
Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama sehemu ya
kuthamini mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi barani Afrika
na pia kukuza ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Namibia na Tanzania,.

Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kuhitimisha ziara yake tarehe 21 Mei, 2025.