Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amesema Serikali kupitia Jeshi la Polisi itagawa magari mapya kwa Wakuu wa Upelelezi wa wilaya (OCCID) nchi nzima ili kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, na kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika katika hali ya amani na usalama.
“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Watanzania kuwa tumejipanga ipasavyo kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa amani na usalama. Tumejipanga kwa vitendea kazi pamoja na utimamu wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuhakikisha kila atakayepanga kufanya fujo anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza hayo leo Mei 21, 2025, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Antipas Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka magari kwa Jeshi la Polisi Malinyi ili liweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Waziri Bashungwa amesema tayari Serikali imeshatoa magari mapya aina ya Land Cruiser kwa wilaya zote za kipolisi ambazo hazikupata magari katika awamu ya kwanza. Pia, kufikia mwezi Agosti 2025, Jeshi la Polisi litasambaza magari mapya kwa Wakuu wa Upelelezi wa wilaya zote nchini.
Wakati akijibu swali la msingi, Waziri Bashungwa amesema Serikali inaendelea kutenga fedha kutoka kwenye bajeti yake kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali yakiwemo magari. Mwezi Septemba 2023, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ilitoa gari jipya kwa wilaya ya Malinyi, hivyo kuifanya wilaya hiyo kuwa na magari mawili yanayofanya kazi.
Leave a Reply