Waajiriwa wapya TRA waonywa kujihusisha na rushwa

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewaonya waajiriwa wapya wa TRA kutojihusisha na vitendo vya Rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na badala yake wachape kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.

Akifunga mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya 1,896 wa TRA katika viwanja vya Gofu Lugalo Jijini Dar es Salaam tarehe 06/06/2025 Kamishna Mkuu Mwenda amesema ni matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa idadi hiyo kubwa ya waajiriwa wapya itakwenda kuleta Mapinduzi TRA kwa kuongeza idadi ya Walipakodi na makusanyo kwa ujumla.

Amesema Mhe. Rais Samia aliamua kuongeza idadi ya waajiriwa wapya 300 na kufikia idadi ya sasa 1896 ili kuwezesha TRA kuendelea kufanya vizuri katika kukusanya Kodi na kuonya kuwa wasije wakajiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa maadili na kuharibu taswira nzuri ya TRA iliyojengwa kwa muda mrefu.

“Kupata kwenu nafasi ya kufanya kazi TRA kumetokana na sifa ya kila mmoja wenu, mtakuwa mashahidi mchakato ulikuwa ni mgumu na makini lengo letu lilikuwa ni kupata watu sahihi na mmepatikana hivyo tunawadai uwajibikaji, iwapo watatokea watakaofanya uvunjifu wa maadili hatutawavumilia, tutawawajibisha bila kujali hali zao, mazingira waliyotoka wala sifa zilizowapa kazi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema ni jukumu la Watumishi wa TRA kuongeza idadi ya Walipakodi kwa kuwasajili Walipakodi wengi zaidi ndiyo maana Serikali imeajiri idadi kubwa ya Watumishi ili wawafikie Walipakodi wengi zaidi katika pembe zote za Tanzania.

“Natarajia mkaongeze utoaji Elimu kwa Umma na Ulipaji Kodi kwa hiari, tekelezeni majukumu yenu mkitambua kuwa Walipakodi ndiyo muhimili mkubwa wa TRA, Wafanyabiashara siyo maadui wa TRA hivyo mnapaswa kuwapatia huduma nzuri na kusikiliza changamoto zao” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wiki mbili kwa Watumishi ambao hawajaripoti kuripoti kazini ili waendelee na majukumu yao la sivyo nafasi zao zitajazwa na Watumishi wengine kutoka kwenye Kanzi Data ya TRA.

Awali Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bw. Moshi Jonathan Kabengwe amesema matarajio ya Uongozi wa TRA kwa waajiriwa wapya hao ni makubwa kwamba watakwenda kuwa na Tija katika utendaji.

Amewataka kila mmoja kuweka juhudi katika kutekeleza majukumu na kuongeza ujuzi na maarifa bila kujali mazingira atakayokuwa anafanyia kazi maana ni jukumu la Mtumishi husika kuongeza thamani yake.

Kwa upande wake Mwakilishi wa waajiriwa wapya Bw. Maximilian Gabriel amesema wapo tayari kufanya kazi katika eneo lolote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.