Lavalava Kuachia Ep Yake Mpya ‘Time’ Agosti Hii.

Msanii mahiri wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, @iamlavalava, ambaye amejijengea jina kupitia midundo na mahadhi ya mapenzi yanayogusa hisia, ametangaza rasmi ujio wa kazi yake mpya — EP inayokwenda kwa jina la “Time”. Kazi hiyo mpya inatarajiwa kuachiwa rasmi Ijumaa hii, tarehe 15 Agosti 2025, hatua ambayo inazidisha hamu kwa mashabiki wake waliokuwa wakisubiri kazi mpya kutoka kwake.

Kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Lava Lava ameweka wazi kuwa EP hiyo ni mkusanyiko wa nyimbo zitakazoakisi safari yake ya kimuziki, mabadiliko ya sauti, na ubunifu mpya ambao amekuwa akiufanyia kazi kwa muda mrefu. Kama sehemu ya kuwapa mashabiki ladha ya kile kinachokuja, ameachia kionjo cha moja ya ngoma zilizopo kwenye EP hiyo ya “Time”, kionjo kilichowasha moto wa shauku miongoni mwa wafuasi wake mtandaoni.

Lava Lava, anayesifika kwa uwezo wake wa kuimba kwa hisia na mitindo mbalimbali, ameahidi kuwa “Time” itakuwa ni moja ya miradi itakayoacha alama katika muziki wa Bongo Fleva mwaka huu. Mashabiki wake sasa wanasubiri kwa hamu siku ya Ijumaa ifike, ili waweze kusikiliza na kuhisi hadithi anazozileta kupitia nyimbo zake mpya.