Paris Saint-Germain wameandika historia baada ya kushinda UEFA Super Cup kwa mara ya kwanza, wakipindua mchezo kwa namna ya kusisimua na kumnyima kocha mpya wa Tottenham, Thomas Frank, taji lake la kwanza akiwa na klabu hiyo.
Mchezo uliofanyika Udine, Italia, ulionekana kuelekea mikononi mwa Spurs baada ya kuongoza 2-0 hadi dakika ya 84. Micky van de Ven alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga mpira uliorudi baada ya jaribio la Joao Palhinha kugonga mwamba, kabla ya Cristian Romero kuongeza bao la pili kwa kichwa dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza.
Lakini PSG, ambao walikuwa wamerudi mazoezini wiki moja tu iliyopita kufuatia kupoteza fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Chelsea mwezi uliopita, walionyesha ari ya kupambana. Lee Kang-in alipunguza tofauti kwa shuti kali kutoka umbali wa yadi 20, na Goncalo Ramos akasawazisha dakika ya 94 kwa kichwa safi kilichowapeleka moja kwa moja kwenye mikwaju ya penalti.

Katika penalti, PSG walianza vibaya baada ya Vitinha kupiga nje, lakini makosa ya Van de Ven (aliyepangua na kipa Lucas Chevalier) na Mathys Tel kupiga pembeni yaliipa nafasi PSG. Nuno Mendes alifunga penalti ya ushindi na kuifanya PSG kushinda 4-3.
Kwa Tottenham, ilikuwa ni pigo kubwa—walikosa nafasi ya kunyanyua kombe lao la pili la Ulaya ndani ya miezi mitatu pekee, baada ya kutwaa Europa League mwezi Mei chini ya Ange Postecoglou, ambaye alifutwa kazi wiki chache baadaye.
Licha ya matokeo, mashabiki wa Spurs wanaweza kufarijika na kiwango kilichooneshwa, hasa kwenye ulinzi, ambapo mfumo wa mabeki watano wa Frank ulizuia PSG kupata shuti la kulenga lango kwa zaidi ya saa moja ya mchezo. Pia, uwezo wao kwenye mipira ya set-piece ulionekana wazi, mabao yote mawili yakitokana na mipira ya adhabu.
Hata hivyo, nguvu ya PSG na uzoefu wao katika michezo mikubwa uliwavuruga Spurs dakika za mwisho, na sasa kikosi cha Frank kinabakiwa na siku tatu pekee kujipanga kwa pambano lao la kwanza la Ligi Kuu England msimu huu dhidi ya Burnley.
Leave a Reply