Baada ya kuahirishwa kwa mchezo wa Derby ya Kariakoo Kati ya Yanga dhidi Simba uliopaswa kupigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa, Machi 8, 2025 kumeibuka mijadala mbalimbali juu ya kuahirishwa kwa mchezo huo.
Mdau wa michezo na Mwanachama wa Yanga, Haji Manara, jana Machi 17, 2025 alinukuliwa akimjibu rais wa Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF), Wallace Karia na kusema kauli za rais huyo ‘zimejaa kiburi na kulewa madaraka’.
Manara aliongea kauli hizo baada ya tamko la Rais wa TFF, Wallace Karia kuzungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa “vitu vingine vinavyofanyika ni vyakijinga, wanaotaka viongozi wa TFF, Bodi ya Ligi kujiuzulu wawaambie viongozi wenyewe wako sawasawa hawastahili kujiuzulu?”.
Baada ya mjadala mrefu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, juu ya kauli ya rais wa TFF, Karia na Manara wa Yanga, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Sc, Ahmed Ally ameibuka kupitia mitandao yake ya kijamii na kusema anayemdhihaki Rais wa TFF ni “MWEHU”.
“Anatokea mwehu mmoja anamdhihaki huyu Rais au kikundi cha vijana wa hovyo wanadhihaki Mamlaka za mpira wetu, Hii Nchi uhuru umepitiliza sana.
“Wallace Karia, TFF na Bodi ya Ligi Wanapaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kutunzwa na kulindwa maana wamefanya kazi kubwa na wanaendelea kufanya kazi kubwa kwenye mpira wetu.
“Yote tuliyokuwa tunayaota kwenye mpira sasa hivi yanatokea, yale tuliyodhani ni magumu kwa Karia yamewezekana, na kama haitoshi tunaiona kesho njema ya mpira wa Tanzania chini ya Karia na wenzake.
Ahmed ameenda mbele na kumtaka Rais wa TFF, Wallace Karia na Uongozi wake wa TFF na Bodi ya ligi kutorudi nyuma na kutokubali mtu kuwarudisha nyuma kwani kwasasa taifa linawaza Kombe la Dunia, AFCON na Ubingwa Afrika ngazi klabu.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.