Aliyekuwa Rais Maskini zaidi duniani afariki

Rais wa zamani wa Uruguay na mwanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kushoto, José “Pepe” Mujica, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.

Taarifa ya kifo chake imetolewa Jumanne na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Yamandú Orsi

Mujica, ambaye alihudumu kama Rais wa Uruguay kati ya mwaka 2010 hadi 2015, aligundulika kuwa na saratani ya koo mwaka 2024. Akiwa madarakani na hata baada ya kung’atuka, Mujica alijizolea umaarufu duniani kwa maisha yake ya unyenyekevu, kiasi cha kutambulika kama “Rais maskini zaidi duniani”.

Tofauti na viongozi wengi, Mujica alikataa kuishi katika Ikulu ya Rais na badala yake aliendelea kuishi katika shamba lake la maua lililoko pembezoni mwa jiji la Montevideo.

Alikuwa akiendesha gari lake la zamani aina ya Volkswagen Beetle, na sehemu kubwa ya mshahara wake akiwa Rais aliitolea misaada kwa mashirika ya kijamii.