Kocha mpya wa Manchester United, Rúben Amorim, amethibitisha wazi kuwa kiungo na nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes, atabakia Old Trafford na ataendelea kuwa sehemu ya msingi katika kikosi chake.
Kauli hii imekuja katikati ya tetesi na uvumi kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo ndani ya klabu hiyo ya Ligi Kuu Uingereza.
Akiwa anazungumza kwa mara ya kwanza kuhusu hatima ya baadhi ya wachezaji wake, Amorim alisisitiza kuwa Bruno ni mchezaji mwenye thamani kubwa, si tu kwa uwezo wake wa kucheza, bali pia kwa uongozi wake na ushawishi mkubwa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.
“Kwa hakika Bruno anabeba jukumu na dhamana kubwa. Yeye ni muhimu sana kwetu,” alisema Amorim kwa msisitizo.
Aidha, Amorim aliongeza kuwa Bruno atakuwa sehemu muhimu mipango yake ndani ya Manchester United, ambao unalenga kuijenga upya timu hiyo ili iweze kurudi kwenye ubora wake wa kihistoria.
“Yeye ni muhimu sana pia kwa kile tunachotaka kukijenga na timu hii,” aliongeza.
Kauli ya Amorim imepokelewa kwa hisia hasa ikizingatiwa kuwa Bruno alikuwa ameonyesha hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake klabuni hapo kufuatia msimu mgumu wa 2024/2025, ambapo United haikuonyesha kiwango cha kuridhisha kwenye mashindano mbalimbali.
Ingawa Bruno mwenyewe aliwahi kusema kuwa hatima yake itategemea maono ya kocha mpya, sasa inaonekana kwamba anabaki kuwa kiungo muhimu katika mipango ya Amorim.
Kwa mashabiki wa Manchester United, hii ni habari njema kwani Bruno ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji thabiti zaidi katika kipindi cha misimu minne iliyopita tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Sporting CP.
Leave a Reply