Arsenal Yaichakaza Real Madrid 3-0 Declan Rice Aibuka Shujaa wa Usiku wa Klabu Bingwa Ulaya

Katika usiku wa kusisimua wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsenal imeibuka kidedea kwa ushindi wa kushangaza wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa watetezi Real Madrid, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Emirates.

Nyota wa kiungo wa Arsenal, Declan Rice, aling’ara kwa kuipatia timu yake mabao mawili ya kiufundi kupitia mipira ya adhabu, akithibitisha ubora wake katika mechi kubwa na kuacha historia ikijirejea kwa namna ya kipekee.

Rice akipiga mpira wa adhabu uliosababisha bao dhidi ya Real Madrid


Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 58, ambapo Rice alichonga mpira kwa ustadi mkubwa na kuupitisha pembeni mwa ukuta wa Real Madrid kabla ya kutua moja kwa moja kwenye kona ya karibu ya goli, huku kipa wa Madrid, Thibaut Courtois, akishindwa kufanya lolote.

Dakika kumi na mbili baadaye, Rice alirejea tena akiwa na utulivu mkubwa na kufunga bao la pili kwa mkwaju mwingine wa adhabu, safari hii akiweka mpira kwenye kona ya juu ya goli, na kuwaacha mashabiki wa Arsenal wakishangilia kwa shangwe isiyoelezeka. Ni kama vile alitaka kumuonesha heshima Roberto Carlos – gwiji wa Madrid aliyekuwa akitazama mchezo huo kutoka jukwaani – ambaye enzi zake alijulikana kwa mipira ya adhabu ya hatari kama hiyo.

Arsenal haikuishia hapo – dakika tano tu baada ya bao la pili, Mikel Merino alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga la tatu, na kuiweka timu hiyo ya London katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009.

Kwa upande wa Real Madrid, licha ya juhudi za kipa wao Courtois ambaye alifanya kazi ya ziada kuzuia mabao zaidi, kikosi hicho kilionekana kushindwa kabisa kupambana na kasi na ubunifu wa vijana wa Mikel Arteta.

Akizungumza baada ya mechi, Declan Rice alisema: “Katika kipindi cha pili tulijua tunahitaji kufunga, na kufunga mabao matatu ni jambo kubwa. Kocha alituambia tuwe na imani ya dhati kuwa tunaweza kushinda mchezo huu, na tukaingia uwanjani tukiwa wamoja na tukiwa na lengo moja.”

Declan Rice akipokea tuzo yake ya mchezaji bora.


Huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kati ya Arsenal na Real Madrid tangu walipokutana mwaka 2006, ambapo Arsenal pia waliibuka na ushindi katika hatua ya 16 bora. Sasa, historia inaonekana kuirudia, huku mashabiki wa Arsenal wakianza kuota ndoto ya kurudi kwenye hatua ya mwisho ya mashindano haya makubwa barani Ulaya.