Baba Wa Asake Adai Kutupwa Na Mwanaye.

Katika video inayosambaa kwa kasi nchini Nigeria, mwanamume anayedaiwa kuwa baba mzazi wa msanii maarufu wa Afrobeat, Asake, ameonekana akiomba msaada kutoka kwa umma. Mzee huyo, anayejulikana kama Mr. Oduns, anasema kuwa anaugua maradhi yanayomfanya mwili wake kupooza na kwamba mwanaye Asake hajakuwa akimsaidia licha ya mafanikio yake makubwa kwenye muziki.

“Wa-Nigeria jamani, mimi ni baba yake Asake. Naombeni msaada, ninaumwa sana na mwili umepooza. Asake hapokei simu zangu, mara ya mwisho kumuona ilikuwa Machi 2022,” alisema mzee huyo kwa huzuni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, inadaiwa kuwa Mr. Oduns alimtelekeza Asake alipokuwa mdogo, hali inayoweza kuwa sababu ya msanii huyo kutokujihusisha naye kwa sasa.

Asake, ambaye kwa sasa anaishi California, Marekani, bado hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu madai haya. Watu mitandaoni wamegawanyika, wengine wakimshutumu kwa kutomhudumia baba yake, huku wengine wakimtetea wakisema huenda ana sababu zake za binafsi za kutofanya hivyo.

Mashabiki na wananchi wanangoja kuona iwapo Asake atatoa majibu rasmi kuhusu suala hili na iwapo atachukua hatua yoyote kumsaidia baba yake.