Bacca wa Yanga apandishwa cheo KMKM, Sasa ni Sajenti

Mchezaji wa Klabu wa ya Yanga, Ibrahim Hamad (Bacca) ambaye ni Askari wa kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar (KMKM) amepandishwa cheo kutoka kuwa Koplo na Sasa amekua Sanjeti wa Jeshi hilo kutokana na utendaji wake uliotukuka katika sekta ya michezo.

Mkuu wa Kikosi cha KMKM, Commodore Azan Msingiri amempandisha cheo hicho leo huku akisema kuwa imani yake kuwa ataendelea kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zake na jeshi la KMKM pamoja na kwenye sekta ya michezo ili kuleta mapinduzi makubwa ya sekta hiyo nchini

Bacca alijiunga na Yanga Januari 14, 2022 akitokea KMKM Uhamisho huu ulifanikishwa baada ya KMKM kumpa likizo ya bila malipo ili aweze kutimiza ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa katika ligi kuu ya Tanzania Bara. 

Tangu ajiunge na Yanga, Bacca ameonyesha kiwango cha juu, akichangia mafanikio ya timu hiyo katika michuano mbalimbali.   

Kutokana na mchango wake mkubwa, Yanga ilimpa mkataba mpya mnamo Novemba 2023, ambao utamuweka klabuni hapo hadi mwaka 2027. 

Rais wa Yanga, Eng. Hersi Said, alieleza kuwa klabu ina mpango wa kuhakikisha Bacca anastaafu akiwa mchezaji wa Yanga, ikionyesha nia ya kumfanya awe sehemu ya klabu kwa muda mrefu.   

Mbali na uchezaji soka, Bacca ni askari katika Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) na alijiunga na jeshi hilo kabla ya kuhamia Yanga na alipata cheo cha Koplo. 

Bacca alianza safari yake ya soka katika klabu ya Jang’ombe Boys mwaka 2017. Baadaye, alijiunga na Malindi SC kabla ya kuhamia KMKM, klabu inayomilikiwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM). 

Akiwa KMKM, aliweza kuonyesha uwezo mkubwa uliomfanya kujulikana zaidi katika medani ya soka nchini.