Bruno akataa donge nono la Hilal, ataka kusalia Ulaya

Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, amekataa rasmi ofa nono kutoka kwa klabu ya Al Hilal inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia (Saudi Pro League), licha ya mshahara wa kuvutia uliokuwa umewekwa mezani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo cha karibu na mchezaji huyo, Fernandes amechukua uamuzi wa kuendelea kucheza soka barani Ulaya, akiamini kuwa ndiko kwenye soka bora zaidi la ushindani wa hali ya juu.

Al Hilal walikuwa wameweka mezani dau kubwa likiwa na mshahara wa mkubwa, wakilenga kumshawishi kiungo huyo mahiri kujiunga nao, lakini Bruno Fernandes alisisitiza kwamba malengo yake ni kuendelea kucheza soka kwenye kiwango cha juu zaidi na kwa sasa hilo lina maana ya kusalia barani Ulaya.

Fernandes, ambaye ni mchezaji muhimu katika safu ya kati ya Manchester United na pia nahodha wa timu hiyo, anaonekana kuweka mbele zaidi masuala ya kiufundi na ushindani kuliko faida za kifedha, jambo linaloonyesha dhamira yake ya kuendelea kutimiza ndoto zake katika soka la juu.