Chama cha ACT Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimelaani vikali shambulio lililofanywa dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, usiku wa Jumatano, Aprili 30, 2025, katika eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Padri Kitima alijeruhiwa kichwani kwa kitu butu na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu. Jeshi la Polisi linamshikilia Rauli Mahabi, mkazi wa Kurasini, kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
Chama cha ACT-Wazalendo kimeeleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kuwa linatoa picha mbaya kuhusu hali ya usalama nchini. ACT Wazalendo imetaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika na vitendo vya aina hiyo kukomeshwa ili kulinda mshikamano na amani ya taifa.
Kwa upande wa CHADEMA, imeeleza kusikitishwa na kulaani vikali shambulio hilo. Chama hicho kilisema kuwa tukio hilo linatisha na linaashiria kuwepo kwa mazingira hatarishi kwa viongozi wa dini na watetezi wa haki.
“Shambulio hili ni ishara ya njama za kuzima sauti za hoja na kueneza hofu kwa walioko mstari wa mbele kudai haki, uhuru na mageuzi ya kweli. Ni jambo lisilokubalika katika taifa linalozingatia misingi ya haki, amani na demokrasia”
“Tunazitaka mamlaka husika zichukue hatua za haraka kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wa tukio hili. Vilevile, Serikali itimize wajibu wake wa kulinda usalama wa viongozi wa dini, wanaharakati na wananchi wote, kwani vitendo vya uvamizi na watu kupotea vimeanza kuzoeleka kwa namna ya kutisha.” – Imeeleza Taarifa iliyotolewa na CHADEMA
Vyama vyote viwili vimetuma salamu za pole kwa Padri Kitima na kumtakia uponyaji wa haraka. Uchunguzi wa polisi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
@Barakadon_
#WasafiDigital
CHADEMA, ACT-Wazalendo walaani tukio la Kushambuliwa kwa Padri Kitima

Leave a Reply