Hadithi ya Andres Escobar imesemwa sana miongoni mwa matukio ya kusikitisha yaliyowahi kutokea katika mchezo wa soka, kwa wale ambao ni wageni na historia hii ni kwamba Escobar alikatishwa uhai wake kwa kupigwa risasi kisa ni bao lake la kujifunga lililochangia Colombia kung’olewa Kombe la Dunia 1994.
Ulimwengu wa soka hadi leo unaumizwa mno kila kumbukumbu hii inapoibuliwa na kalamu za waandishi kama ilivyo katika andiko hili, kwa sababu makosa ya timu nzima ya Colombia hadi kuondolewa mashindanoni yaliangukia kwa Escobar na hatima yake ikawa ni kifo.
Ukweli ni kwamba mwanasoka huyo alifanyiwa ukatili usio na sababu za msingi, kwa sababu hiyo muuaji wa Escobar aliyejulikana kwa jina la Humberto Muñoz Castro alikutana na hukumu ya miaka 43 jela kabla ya kuachiwa huru mwaka 2001.
Mabosi wa muuaji, ‘The Gallon Henao brothers’ wao waliepuka kifungo kwa kisingizio cha uhaba wa ushahidi lakini ukweli ulikuwa ni huu; serikali ya Colombia ilizidiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya magenge ya kihalifu nchini Colombia enzi hizo hivyo mauaji yanayofanana na Escobar kilikuwa ni kitu cha kawaida sana.
Kama Escobar angebarikiwa bahati ya kuendelea kuishi ni wazi kabisa angesahihisha kosa lake. Kwa bahati mbaya kifo kilimfikia haraka sana na kumnyima hata nafasi ya kucheza AC Milan ambao walikuwa mbioni kumsajili kabla ya mauti kumkuta.
Kufuatia ukatili aliofanyiwa Escobar, jiji la Medellin pale Colombia alikouwawa beki huyo lilizindua sanamu kwa ajili ya kuyaenzi maisha yake mafupi katika mchezo wa soka. Kwamba Escobar aliyeonekana msaliti, leo hii ni shujaa kwa Wacolombia.
Huku kwetu, habari ya jiji hivi sasa ni Ladack Chasambi ambaye ameibuka kuwa shujaa baada ya lile tukio lake la kujifunga dhidi ya Fountain Gate na kuigharimu Simba alama mbili muhimu.
Ushujaa wa Chasambi umekuja vipi? Ni baada ya kutupia wavuni bao moja na kuiwezesha Simba kuchomoza na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons mapema wiki hii.
Ndani ya siku chache sana Chasambi amekuwa ni chanzo cha mabadiliko ya hisia za mashabiki wa Simba kutoka kuwa ni wenye hasira na machungu hadi kuwa na furaha isiyoelezeka.
Chasambi asingeweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo uliofuata baada ya ule wa Fountain Gate kama asingepata msaada mkubwa kutoka benchi la ufundi la Simba chini ya kocha Fadlu Davis ambaye anaamini klabu hiyo ni familia kubwa, inayotakiwa kuishi katika umoja hasa katika nyakati hizi ambazo Simba wanalisaka kombe la Ligi Kuu kwa udi na uvumba.
Hivyo ndivyo taasisi za michezo zinavyofanya kazi. Kwa maana makosa katika michezo ni kitu kinachowezekana na ambacho kinawezekana zaidi ni kwamba mchezaji ana uwezo wa kuendelea kucheza iwapo tu; ATAKUBALI MAKOSA na KUONGEZA UMAKINI kama ilivyotokea kwa Chasambi na Simba.
Waliomuua Escobar hawakujua kwamba mchezaji huyo angefanya kila linalowezekana kufuta kumbukumbu mbaya aliyowapa katika fainali za Kombe la Dunia 1994 kama Chasambi alivyosuuza mioyo ya Wanasimba baada ya kujifunga dhidi ya Fountain Gate.
Bahati nzuri Chasambi hayupo katika mazingira ya Colombia. Hawezi kukutana na ukatili aliofanyiwa Escobar. Alichokutana nacho ni maneno tu na sio risasi ambayo ingemfuta katika historia ya dunia.
Na binafsi nampongeza Chasambi kwa ukomavu wake wa akili ndani ya kipindi kifupi kilichotenganisha mechi ya Fountain Gate na hii ya Tanzania Prisons. Kujitokeza mstari wa mbele hasa kwa hawa mashabiki wa Simba na Yanga na kujitutumua hadi kusawazisha makosa sio jambo jepesi.
Hata kazi ya benchi la ufundi Simba imekuwa ni rahisi katika kuhakikisha Chasambi haanguki zaidi kwa sababu mchezaji mwenyewe amekubali alikosea, ameendelea kutimiza jukumu lake uwanjani na ameboresha kutoka kutumbukiza boli kwenye nyavu zake na kuweka katika nyavu za wapinzani.
Makosa hayakwepeki katika uwanja wa michezo. Soka pekee limezalisha matukio mengi ya wachezaji kukosea hatua fulani za matendo yao na sio tu bal la kujifunga la Escobar hadi kupelekea kifo chake.
John Terry aliteleza wakati anapiga penati fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester United mwaka 2008 na kuinyima Chelsea kombe. Baada ya hapo Terry hakuinamisha kichwa chini, alikubali kosa na akaendelea kufanya vyema sana Stamford Bridge.
Oliver Khan alikuwa mzembe fainali ya Kombe la Dunia 2002 dhidi ya Brazil ya Ronaldo de Lima huku yeye akiwa ndiye golikipa tegemeo Ujerumani. Hakujificha chumbani kwake na kulia bali aliendelea kusonga mbele kama nahodha.
David Beckham aliigharimu England kwa kuoneshwa kadi nyekundu ya kizembe mno dhidi ya Argentina mwaka 1998, alipata wakati mgumu sana mwanzoni kupambana na lawama lakini alikaza buti na baada ya hapo alinyakua takribani makombe 10 katika klabu tofauti alizozitumikia.
Wakati Escobar akinyimwa nafasi ya kusahihisha kosa lake na kuishia kuuwawa, hadithi ni tofauti kwa Terry, Khan, Beckham na Chasambi. Hadithi ya mashujaa waliokubali uhalisia na kuishi nao. Kudos!
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.