Dili la De Bruyne kutua Napoli lafikia pazuri

Mawakili wa mchezaji nyota wa Manchester City, Kevin De Bruyne, wanatarajiwa kuwasili mjini Napoli ndani ya saa chache zijazo kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo ya mwisho kuhusu mkataba wa miaka mitatu.

Hatua hii inakuja baada ya pande zote mbili yaani Kevin De Bruyne na klabu ya Napoli kuonyesha nia ya kufanikisha uhamisho huu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na mazungumzo haya, Napoli wana matumaini makubwa kwamba makubaliano hayo yatakamilika ndani ya saa 48 zijazo.

Hii inaashiria kuwa pande zote ziko katika hatua za mwisho na tofauti yoyote iliyobaki inatarajiwa kufutwa na mawakili hao watakapokutana ana kwa ana na maafisa wa Napoli.

Iwapo dili hili litakamilika kama ilivyopangwa, itakuwa ni hatua kubwa kwa Napoli, kwani Kevin De Bruyne ni mmoja wa viungo bora kabisa duniani, akiwa na uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu ya England na pia mashindano ya kimataifa akiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji.

Ujio wake unaweza kuimarisha kwa kiasi kikubwa kikosi cha Napoli, hasa ikizingatiwa kwamba wanashiriki mashindano ya ndani na ya kimataifa.

Kwa upande wa Manchester City, kama dili litatimia, huu utakuwa mwisho wa enzi kwa mmoja wa wachezaji waliokuwa muhimu sana katika mafanikio ya timu hiyo chini ya kocha Pep Guardiola. Hii pia inaweza kuashiria mabadiliko ya kizazi ndani ya kikosi hicho.