Dkt. Mpango ashiriki uapisho wa Rais Mpya wa Ghana

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, leo Jumanne, Januari 7, 2025, ameshiriki katika hafla ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Ghana, John Dramani Mahama. Hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Independence Square, jijini Accra, Ghana.

Dk Mpango alimpongeza Rais Mahama kwa ushindi wake na kumtakia mafanikio katika uongozi wake mpya. Mahama ameapishwa kuwa Rais wa Ghana, akichukua nafasi ya Nana Addo Akufo-Addo, aliyemaliza muda wake wa uongozi.

John Dramani Mahama alichaguliwa kuwa Rais wa Ghana baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 7, 2024. Mahama, aliyewakilisha Chama cha National Democratic Congress (NDC), alimshinda mpinzani wake, Mahamudu Bawumia, aliyekuwa Makamu wa Rais na mgombea wa chama tawala cha New Patriotic Party (NPP).

Hii ni mara ya pili kwa Mahama kushika wadhifa huo, kwani aliwahi kuwa Rais wa Ghana kati ya mwaka 2012 na 2017. Ushindi wake umepongezwa na viongozi wa ndani na wa kimataifa kama ishara ya imani kubwa ya wananchi wa Ghana katika uongozi wake.

Hafla ya kuapishwa kwa Rais Mahama imehudhuriwa na viongozi wa mataifa mbalimbali, wakiwemo marais, mawaziri, na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, ikiwa ni ishara ya mshikamano wa kikanda na kimataifa kwa Ghana.