Rais wa heshima na Mwekezaji wa Simba Sc, Mohamed Dewji kupitia taarifa yake ameeleza kuwa anaamini mechi yao ya fainalai ya Kombe la Shirikisho Afrika kuhamishiwa visiwani Zanzibar ni kutotendewa haki kwani uwanja wa Benjamin Mkapa ulishatimiza matakwa yote yaliyopendekezwa na CAF ili fainali hizo zipigwe Benjamin Mkapa.
“Ndugu zangu Wanasimba, nawaandikia leo nikiwa na masikitiko, lakini pia nikiwa na imani isiyotetereka.
Katika wiki chache zilizopita, tumeshirikiana kwa karibu na taasisi husika kuhakikisha tunapata haki stahiki: fursa ya kuandaa mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF katika Uwanja wetu wa Benjamin Mkapa.
“Kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa, kila hatua ya ukarabati wa uwanja ilifuatwa kwa umakini ili kuhakikisha unakuwa tayari kwa mechi hiyo ya fainali.
“Wakati huohuo, baadhi ya matukio yaliyotokea nyuma ya pazia yameacha maswali ya msingi. Taarifa zilianza kusambaa mtandaoni kabla ya taarifa rasmi kutolewa. Tulieleza wasiwasi wetu kwa uwazi.
“Pamoja na juhudi hizi zote, CAF imethibitisha kuendeleza vamuzi wa kuhamishia fainali hiyo Zanzibar.
“Bila shaka, matokeo haya ni ya kusikitisha – si kwa Simba tu, bali kwa mashabiki wetu, na kwa wote waliotoa juhudi kubwa kuandaa tukio hili katika historia ya Simba Tanzania.
Kwa mtazamo wangu wa binafsi, hatukutendewa haki.
“Lakini nasema pia: hatujakata tamaa.
Simba haijawahi kuwa klabu inayotegemea mazingira ya faraja. Tunastawi chini ya shinikizo – tukiendeshwa na imani, na nguvu ya watu wetu.
“Tunaenda Zanzibar si kwa hiari – bali kwa wajibu. Na tutatimiza wajibu huo kwa mshikamano, kwa dhamira, na kwa fahari – yaliyosalia tunamwachia Mwenyezi Mungu.
“Kwa wachezaji wetu: mnavaa nembo yenye historia. Ingieni Amaan kwa vichwa juu. Chezeni kwa ujasiri, kwa umakini na kwa utulivu – kama mashujaa wa Simba mlivyo.
“Kwa mashabiki wetu: naelewa hisia zenu. Nami pia nahisi hivyo. Lakini sasa ni wakati wa kugeuza hisia hizo kuwa nguvu ya pamoja. Tujaze Amaan kwa moyo, kwa matumaini, na kwa sauti. Tuwafanye wapinzani wetu waone na wasikie kishindo cha Simba – popote tulipo.
“Asante kwa wadau wote waliowezesha safari hii – serikalini, shirikisho la mpira, vyombo vya habari, na kila aliyeshiriki katika maandalizi ya mchezo huu.
“Na kwa wote mnaotazama: uwanja unaweza kuwa umebadilika, lakini Simba ni yule yule.
Dhamira yetu iko wazi: tunaelekea Zanzibar tukiwa tayari kupambana.
Simba ni Mfalme. Na anaweza kunguruma popote.
Leave a Reply