Hersi Aeleza Yaliyojadiliwa Katika Kikao na Waziri Kabudi Kuhusu Kariakoo Dabi

Hersi Aeleza Yaliyojadiliwa Katika Kikao na Waziri Kabudi Kuhusu Kariakoo Dabi

Mjadala kuhusu hatma ya mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Yanga na Simba bado unaendelea, huku Young africans s.c ikiendelea kushikilia msimamo wake wa kutocheza mechi hiyo upya na badala yake kudai pointi tatu. Kutokana na mgogoro huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, aliitisha kikao maalum kilichohusisha viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), pamoja na klabu za Yanga na Simba, ili kujadili njia bora ya kutatua sintofahamu hiyo.

Yanga Yatoa Msimamo Wake Baada ya Kikao

Kikao cha kwanza kilifanyika Alhamisi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo viongozi wa Yanga walikuwa wa kwanza kuwasilisha maoni yao mbele ya Waziri na timu yake.

Baada ya kutoka kikaoni saa 9:21 alasiri, viongozi wengi wa Yanga waliepuka kuzungumza na vyombo vya habari, wakimwachia Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, kutoa taarifa rasmi.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Hersi alisema kuwa walipata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa Waziri na timu yake, huku wakisisitiza kuwa msimamo wa Yanga ni kusimamia maslahi ya klabu na wanachama wake.

“Tumepata nafasi ya kukutana na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa. Katika mazungumzo haya, tumeweza kueleza msimamo wa Yanga kuhusu mchezo wa Kariakoo Dabi,” alisema Hersi.

Aliongeza kuwa Waziri Kabudi alisisitiza kuwa kikao hicho hakikuwa cha kufanya maamuzi, bali kililenga kupata suluhu kwa kusikiliza pande zote zinazohusika.

“Tumewasilisha hoja zetu kwa kina, na Waziri pamoja na timu yake wametuelewa. Tumekubaliana kuwa vikao vitaendelea ili kupata muafaka wa jambo hili,” aliongeza.

Aliongeza kuwa Waziri Kabudi alisisitiza kuwa kikao hicho hakikuwa cha kufanya maamuzi, bali kililenga kupata suluhu kwa kusikiliza pande zote zinazohusika.

“Waziri amekubali kuwa hawezi kufanya maamuzi bali anasikiliza na kutafuta suluhisho. Alisema kikao hiki ni kwa ajili ya kufahamu nini kinatoka kwa viongozi wa Yanga na si kufanya maamuzi ya sakata hili kwa haraka,” alifafanua Hersi.

“Tumewasilisha hoja zetu kwa kina, na Waziri pamoja na timu yake wametuelewa. Tumekubaliana kuwa vikao vitaendelea ili kupata muafaka wa jambo hili,” aliongeza.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao zinaeleza kuwa Yanga imesisitiza msimamo wake wa kutocheza mechi hiyo upya na badala yake wanataka pointi tatu kwa mujibu wa kanuni.

Simba Yafanya Mazungumzo na Waziri

Baada ya kikao cha Yanga kumalizika, viongozi wa Simba waliingia kikaoni saa 9:23 alasiri kwa mazungumzo yao na Waziri Kabudi. Ingawa maudhui ya kikao hicho hayakufafanuliwa kwa kina, viongozi wa Simba walisisitiza kuwa walijadili masuala mapana ya maendeleo ya soka nchini badala ya kujikita moja kwa moja kwenye mchezo dhidi ya Yanga.

Baada ya kikao hicho, viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi walialikwa kwa mazungumzo yao ili kutoa mtazamo wa mamlaka hizo kuhusu mgogoro huo.

Mashabiki wa Yanga Wapongeza Viongozi Wao

Baada ya kutoka kikaoni, mashabiki wa Yanga waliokusanyika nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa walishangilia walipowaona Hersi Said na Makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji wakitoka.

Katika mazungumzo mafupi na mashabiki hao, Hersi aliwataka kuwa watulivu huku wakisubiri uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya mchezo huo.

“Wananchi eeeh! Mko sawa? Nyie mlituchagua kuisimamia Yanga. Asanteni,” alisema Hersi, akionekana kuwa na imani kwamba uongozi wa Yanga unafanya kazi yake kwa weledi mkubwa.

Kwa sasa, mashabiki wa soka wanabaki kusubiri maamuzi ya mwisho kutoka kwa mamlaka husika kuhusu iwapo mechi hiyo itapangiwa tarehe mpya au la.