Hizi hapa rekodi za wapinzani wa Tanzania AFCON 2025

NA KELVIN LYAMUYA

BAADAE mnamo majira ya Saa 3 usiku, Watanzania watakuwa makini kufuatilia zoezi la kupanga makundi ya fainali za AFCON 2025 ambazo zitafanyika nchini Morocco na kushirikisha jumla ya timu 24.

Tanzania ni moja kati ya timu hizo 24 zilizofanikiwa kufuzu kushiriki AFCON 2025, ikiwa katika ‘pot 4’ sambamba na timu za Msumbiji, Comoro, Sudan, Zimbabwe na Botswana.

Timu hizo sita ni sawa na nyingine 18 ambazo nazo zimegawanywa katika ‘pot’ nyingine 1, 2 na 3 ambapo ‘pot 1’ ina Morocco, Senegal, Misri, Ivory Coast, Nigeria na Algeria.

Cameroon, Mali, Tunisia, Afrika Kusini, DR Congo na Burkina Faso zipo katika ‘pot 2’ wakati Gabon, Angola, Zambia, Uganda, Guinea ya Ikweta na Benin zikimiliki ‘pot 3’.

Na hizi ndio rekodi za timu zote zinazotarajiwa kupambania kombe katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya kitaifa Barani Afrika.

POT 4

TANZANIA (Viwango FIFA #106)

-Ni mara yao ya 4 kushiriki AFCON (1980, 2019, 2023 na 2025)
-Hawajawahi kuvuka hatua ya makundi

MSUMBIJI (Viwango FIFA #96)

-Fainali za 2025 ni za sita kwao baada ya 1986, 1996, 1998, 2010 na 2023
-Mwaka huu wamerudia rekodi yao ya kufuzu mara mbili mfululizo, kama walivyofanya 1996 na 1998 wamerudia tena 2023 na 2025.

COMORO (Viwango FIFA #103)
-Wanashiriki fainali hizo kwa mara ya pili baada ya zile za 2021 ambazo waliweka rekodi ya kufika hatua ya 16 Bora kama ‘best looser’ baada ya kuwafunga Ghana 3-2 licha ya kupoteza mechi 2 za awali

SUDAN (Viwango FIFA #113)
-Mabingwa wa AFCON 1970 kabla ya kupitia anguko kubwa la kiufundi lililowaondoa katika ramani ya Soka Afrika kuanzia 1976 hadi 2008
-Urejeo wao wa nguvu 2012 uliwavusha hadi Robo Fainali na baada ya hapo walipotea tena hadi 2021.

ZIMBABWE (Viwango FIFA #121)
-Watashiriki AFCON ya mwaka huu kwa mara ya sita baada ya 2004, 2006, 2017, 2019 na 2021
-Hawajawahi kuvuka hatua ya makundi

BOTSWANA (Viwango FIFA #136)
-Zaidi ya kushiriki Raundi ya Kwanza katika hatua za kufuzu 2012, Botswana hawana rekodi nyingine ya kutisha.

POT 3

GABON (Viwango FIFA #84)

-Watashiriki fainali hizo kwa mara ya 9 huku wakiwa na rekodi ya kuvuka hatua ya makundi mara 3
-Waliweza kushiriki hatua ya Robo Fainali 1996 na 2012, bila kusahau hatua ya 16 Bora 2021

ANGOLA (Viwango FIFA #85)

-Kwenye rekodi zao, fainali za AFCON 2025 zinasomeka kuwa ni za 10 katika ushiriki wao baada ya kufanya hivyo 1996, 1998, 2006, 2008, 2010, 2012, 2013, 2019 na 2023
-Baada ya kuvuka hadi Robo Fainali katika michuano ya 2008, 2010 na 2023, Angola hawana rekodi nyingine ya kutisha katika matoleo mengine ya AFCON.

ZAMBIA (Viwango FIFA #87)
-Historia inaonesha Zambia walishashiriki fainali hizo mara 18 na mwaka huu ni ya 19 na kabla ya fainali hizi za 2025, Zambia pia waliweka rekodi ya kuvuka hatua ya makundi mara 8.
-Juhudi zao ziliwawezesha kutinga Robo Fainali 1992 na 2010, Mshindi wa Pili 1974 na 1994, Mshindi wa Tatu 1982, 1990 na 1996 na ubingwa ambao waliutwaa 2012

UGANDA (Viwango FIFA #88)

-Baada ya kutia saini zao katika matoleo 7 ya Afcon, Uganda watashiriki fainali za 8 wakiwa na lengo la kufika mbali zaidi.
-Mwaka 1962 waliishia kuwa washindi wa 4 na 1978 wakasogea zaidi hadi washindi wa 2 kabla ya kugota hatua ya 16 Bora kwenye mashindano ya 2019.

GUINEA IKWETA (Viwango FIFA #93)

-Wameshiriki fainali za AFCON mara 4 na zote walivuka hatua ya makundi, wakitambia rekodi za kucheza hatua ya Robo Fainali 2012 na 2021, Raundi ya 16 Bora 2023 na Mshindi wa Nne 2015

BENIN (Viwango FIFA #94)

-Katika majaribio yao manne ya kupambania Kombe la AFCON, Benin waliweza kuvuka hatua ya makundi mara moja tu (2019) huku fainali za 2004, 2008 na 2010 zote wakiishia ‘group stage’
-Fainali za mwaka huu ni za 5 kwao na wanatarajiwa kujaribu kuvunja rekodi yao ya kucheza Robo Fainali 2019.

POT 2

CAMEROON (Viwango FIFA #49)

  • Moja ya timu vigogo Afrika ikiwa na rekodi ya kutia saini mara 21 katika fainali za AFCON na mwaka huu ni ya 22!
    -Rekodi safi ya Cameroon ni ya kubeba ubingwa katika fainali tano (1984, 1988, 2000, 2002 na 2017).

MALI (Viwango FIFA #51)

-2008, 2010, 2015 na 2017 ndio miaka ambayo Mali walishindwa kuvuka makundi ya AFCON lakini 1972 walitoboa hadi kuwa Washindi wa Pili
-Mafanikio yao mengine ni kuwa Washindi wa Nne (1994, 2002, 2004), Washindi wa Tatu (2012, 2013), Hatua ya 16 Bora (2019, 2021) na Robo Fainali 2023.

TUNISIA (Viwango FIFA #52)

-Jumla ya fainali walizoshiriki Tunisia hadi sasa ni 22 (kabla ya hii ya 2025), wakibeba kombe moja tu 2004 ambapo walikuwa ndio wenyeji
-Wana rekodi ya kuwa Washindi wa Nne (1978, 2000, 2019), Washindi wa Tatu (1962), Washindi wa Pili (1965, 1996) na Robo Fainali mara 7 (1998, 2006, 2008, 2012, 2015, 2017, 2021)

AFRIKA KUSINI (Viwango FIFA #57)

-Moja ya timu zilizoshiriki AFCON mara nyingi pia ni hii kutoka kwa Madiba. Fainali za 2025 ni za 12 kwa Afrika Kusini, wakiwa na rekodi ya kubeba kombe hilo mara moja (1996)
-Pia wana rekodi ya kumaliza Washindi wa Tatu (2000 na 2023) na Washindi wa Pili 1998.

DR CONGO (Viwango FIFA #61)

-Katika jumla ya mashindano 20 ya AFCON ambayo Congo DR wameshiriki, mawili kati ya hayo waliweza kuchomoza na ubingwa (1968 na 1974)
-1972 na 2023 walimaliza Washindi wa Nne huku 1998 na 2015 wakimaliza Washindi wa Tatu.

BURKINA FASO (Viwango FIFA #66)

-Katika fainali 3 za AFCON walizoshiriki hivi karibuni, Burkina Faso waliweza kumaliza kama Washindi wa Pili na Tatu kwa kuzifunga Nigeria 2013 na Ghana 2017.

POT 1

MOROCCO (Viwango FIFA #14)

-Wana rekodi ya kubeba kombe moja tu la AFCON (1976) katika jumla ya majaribio yao 20 ya kupambana katika michuano hiyo.
-Mara mbili walimaliza Washindi wa Nne (1986, 1988), Washindi wa Tatu (1980) na Washindi wa Pili (2004)

SENEGAL (Viwango FIFA #17)

-2021 ndio mwaka ambao Senegal walifanikiwa kuvaa medali ya Ubingwa wa AFCON ndani ya matoleo 17 tofauti ya michuano hiyo
-1965, 1990 na 2006 waliweka rekodi ya kuwa Washindi wa Nne na pia wakawa Washindi wa Pili 2002 na 2019.

MISRI (Viwango FIFA #33)

-Wameshiriki jumla ya fainali 26 za AFCON na kwa ufupi tu, hawa ndio mabingwa wa kihistoria wakiwa na medali zao 7 walizotwaa 1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010.

IVORY COAST (Viwango FIFA #46)

-Wameshiriki fainali za AFCON mara 25 na ndio mabingwa watetedi wa mashindano hayo waliyotwaa kwa mara ya tatu mwaka 2023, 2015 na 1992.

NIGERIA (Viwango FIFA #44)

-Katika fainali hizi za 21 kwao, Nigeria wanatazamia kuongeza taji la nne la AFCON baada ya yale ambayo waliyatwaa 1980, 1994 na 2013.

ALGERIA (Viwango FIFA #37)

-Mabingwa hawa wa 1990 na 2019 watashiriki fainali zao za 21 mwaka huu wakiwa katika ardhi ya wapinzani wao.