Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekanusha uvumi unaoenea mitandaoni ukidai kuwa mfumo wa uchaguzi umeunganishwa na mifumo mingine kama vile Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na chama fulani cha siasa, pamoja na madai kwamba zoezi la kupiga kura tayari limekamilika.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa leo na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima, INEC imeeleza kuwa madai hayo si ya kweli na kwamba ni upotoshaji wenye lengo la kuwatia hofu wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025
Tume hiyo imesisitiza kuwa hakuna mfumo wa kielektroniki unaotumika katika hatua yoyote ya mchakato wa uchaguzi iwe ni upigaji kura, kuhesabu kura, au kutangaza matokeo.
Uchaguzi unafanyika kwa njia ya kawaida (manual) ambapo kila mpiga kura hutambulishwa kupitia Kadi ya Mpiga Kura iliyotolewa na INEC pekee. Aidha, Kitambulisho cha Taifa (NIDA) hakitumiki katika mchakato huo.
INEC imeongeza kuwa baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura vyama vyote vya siasa vilipatiwa nakala zake ili kuhakikisha uwazi na ushirikishwaji wa pande zote. Katika siku ya kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa hushirikiana na wasimamizi wa vituo kuthibitisha majina ya wapiga kura kupitia daftari hilo, hivyo kuthibitisha kuwa mchakato huo hauna uhusiano wowote na mifumo ya siri au ya kiteknolojia ya nje.
INEC imewataka wananchi kuwa watulivu na kupuuza taarifa zinazotolewa nje ya vyanzo rasmi, huku ikisisitiza kuwa taarifa sahihi kuhusu uchaguzi zitapatikana kupitia tovuti yake rasmi ([www.inec.go.tz](http://www.inec.go.tz)) pamoja na kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Tume pia imetoa onyo kali kwa watu wanaosambaza taarifa za upotoshaji, ikisema kuwa hatua hiyo inalenga kuleta taharuki katika jamii.
INEC imehimiza wananchi kuwapuuza watu wa aina hiyo na kujiandaa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao.
INEC yakanusha Upotoshaji Mfumo wa uchaguzi kuunganishwa na mifumo mingine

Leave a Reply