Mac Miller Aweka Rekodi Mpya Miaka 6 Baada Ya Kifo Chake .

Marehemu rapa Mac Miller ameendelea kung’ara baada ya albamu yake #Balloonerism kujinyakulia nafasi ya kwanza kwenye chati mbalimbali za Billboard, zikiwemo Top Album Sales, Top Rap Albums, Vinyl Albums, na Indie Store Album Sales. Albamu hii, iliyorekodiwa tangu 2014 lakini ikacheleweshwa, imeuza nakala zaidi ya 41,000 Marekani – rekodi bora zaidi ya Miller..

Kwenye Billboard 200, Balloonerism imeingia nafasi ya tatu, ikiwa albamu yake ya nane kufika Top 10. Pia, nyimbo saba kutoka kwenye albamu hiyo zimeingia kwenye chati ya Hot R&B/Hip-Hop Songs, huku “Funny Papers” ukishika nafasi ya 16, ukiwa wimbo wake wa pili kufika juu zaidi kwenye chati hiyo baada ya “Good News” (2020) kufika nafasi ya 10.

Mafanikio haya pia yamempeleka Mac Miller hadi nafasi ya pili kwenye *Billboard Artist 100, ikiwa ni rekodi yake ya juu kabisa kwenye chati hiyo. Hii ni takribani miaka sita na miezi minne baada ya kifo chake kilichotangazwa Septemba 7, 2018, jambo linalodhihirisha upendo mkubwa wa mashabiki kwa kazi zake hata baada ya kuondoka duniani.