Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar zitaendelea kusimamia kwa dhati na kwa haki misingi ya demokrasia na
kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi kwa
uhuru, kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye
sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani
Pwani. Ametoa wito kwa wananchi wote hususan vijana kuwa waangalifu na watu
wasioitakia mema nchi kwa kuepuka kutumiwa vibaya kufanya vitendo vya uvunjifu
wa amani.

Makamu wa Rais amesema Wadau wote wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa
wanahimizwa na kukumbushwa kuwa wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha
kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu, kwa kuendesha kampeni
zenye staha na kuzingatia Sheria na miongozo mbalimbali ya uchaguzi. Ameongeza
kwamba Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 42(2) na 65, Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya
Mwaka 2024 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi
ya Zanzibar Na. 4 ya mwaka 2018.
Halikadhali Makamu wa Rais ameagiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ili
waweze kutekeleza jukumu la kizalendo walilokabidhiwa la kuhakikisha kuwa
wanawafikia wananchi na kuwapa taarifa sahihi kuhusu sera, mipango, miradi na
mikakati ya Serikali katika kuwaletea Maendeleo.

Vilevile Makamu wa Rais amesema Mbio za Mwenge pamoja na mambo mengine
zitaangazia masuala ya lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano
dhini ya VVU na UKIMWI, mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Makamu wa Rais amesema wazo la kukimbiza mwenge wa uhuru nchi nzima na kila
mwaka lilitolewa na Vijana wa TANU katika kikao chao kilichofanyika tarehe 26 Juni, 1964 Lengo kuu likiwa ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Baba wa Taifa ya
kuhamasisha umoja, upendo, amani na ujenzi wa Taifa kwa kuhamasisha
maendeleo. Tangu wakati huo, mwenge umekuwa ukikimbizwa katika maeneo
mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kupitia mbio hizo
hamasa kubwa imetolewa ili kuendelea kudumisha amani, na kujenga uzalendo,
umoja na mshikamano. Katika kipindi chote hicho, mbio za mwenge zimekuwa na
mafanikio makubwa yanayosadifu maono ya waasisi wa Taifa letu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 zinabeba kauli mbiu isemayo
“Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na
Utulivu” ambayo inalenga kuwakumbusha na kuwasisitiza Watanzania wote kutumia
kikamilifu haki yao ya kikatiba ya kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.
Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 unatarajiwa kukimbizwa kwa muda wa siku
195, katika Mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Serikali
itafikisha ujumbe kwa wananchi na kuhamasisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali
za maendeleo kwa kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi
katika miradi ya maendeleo.

Uzinduzi wa Mbio za Mwenge kwa Mwaka 2025 umehudhuriwa na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Dotto Biteko, Rais Mstaafu wa Awamu
ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu,
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said,
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Viongozi
wa Mahakama, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa
Vyama vya Siasa pamoja na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Leave a Reply