Mbeya City yawasha taa ya kijani, kurejea Ligi Kuu kwa kishindo

Klabu ya Mbeya City imewasha taa ya kijani kurejea Ligi Kuu ya NBC 2025/2026 baada ya kuichapa Kiluvya FC kichapo cha mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Championship ya NBC (Ligi Daraja la Kwanza) uliopigwa leo Machi 17, 2025 katika Dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Ushindi huo umezidi kuimarisha nafasi nafasi ya Mbeya City katika msimamo wa ligi, ambapo wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 49 katika michezo 23 waliocheza.

Msimu huu, Mbeya City imeonyesha maendeleo makubwa chini ya kocha wao, Salum Mayanga, ambaye alichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi Desemba baada ya kuiongoza timu kushinda michezo mitatu mfululizo na kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi.  

Klabu ya Mbeya City ilianzishwa mwaka 2011 na ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2013. Tangu wakati huo, timu imekuwa ikishiriki katika ligi hiyo kwa mafanikio tofauti.

Katika msimu wa 2022/2023, Mbeya City ilikabiliwa na changamoto kubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Timu ilipambana kuhakikisha inabaki kwenye ligi kuu, lakini matokeo hayakuwa mazuri.

Kufuatia matokeo hayo, Mbeya City ilishuka daraja na kushiriki Ligi ya Championship katika msimu wa 2023/2024.  

Katika msimu huu wa 2024/2025, Mbeya City m inaendelea kupambana ili kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara na timu hiyo imeonyesha maendeleo mazuri, ikiwa miongoni mwa timu zinazofanya vizuri katika ligi hiyo.