Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Steven Mguto, amesema kuwa iwapo wao kama mamlaka za mpira watashindwa kutatua sakata la mechi kati ya Simba na Yanga, ambayo haikufanyika Machi 8, 2025, basi wataishirikisha Serikali ili kusaidia kupata suluhisho.
Kauli hiyo inakuja baada ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo huo wa Derby ya Kariakoo, huku Yanga ikiandika barua ikieleza kuwa hawatacheza tena mchezo huo na kudai alama tatu.
“Jambo hili likitushinda kabisa lazima tuihusishe Serikali iweze kusaidia, kwa sababu kuhakikisha amani inakuwepo sio suala letu sisi peke yetu – kila mtu anatakiwa kuhakikisha kuwa kuna amani,” amesema Mguto.
Mguto aliongeza kuwa kuziongoza timu kubwa kama Simba na Yanga si jambo rahisi kutokana na ukubwa wa mashabiki na umuhimu wa klabu hizo kwenye soka la Tanzania.
“Nikubali kuwa tunaongoza timu ambazo zina umaarufu mkubwa, hakuna mtu anayeweza kukataa. Ndiyo maana unaona tunasumbuka kukaa vikao hapa na pale. Kama ingekuwa rahisi, tungeenda moja kwa moja kusema, ‘wewe umefanya hiki, faini yako ni hii’ au ‘wewe umefanya hiki, unashushwa daraja.’
“Piga picha umeishusha Yanga daraja, umeishusha Simba daraja. Ni kwa sababu tumekuwa na malezi mabaya tangu huko nyuma, sasa ni tatizo kubwa sana kurekebisha mambo sasa hivi,” alisema Mguto.
Akitolea mfano kesi zilizowahi kutikisa Bodi ya Ligi, Mguto alikiri kuwa kesi ngumu zaidi kufanyiwa maamuzi ilikuwa ya mwaka 2021, ambapo Yanga waligoma kucheza mechi baada ya muda wa kuanza kwa mchezo huo kusogezwa mbele.
“Kesi iliyowahi kutusumbua kuifanyia maamuzi ni ile ya Yanga ya mwaka 2021, walipogoma kucheza baada ya muda wa mechi kusogezwa mbele. Ile kesi ilitusumbua sana, afadhali ya hii maana ilikuwa karibu kupelekea mtu kukatwa alama tatu.
“Anapogomea mtu na ni muda wa mechi, na marefa wako uwanjani na wakafanya taratibu zote, hiyo unakuwa huna jinsi – sheria inapaswa kuchukua mkondo wake.
“Lakini bahati nzuri tuliamua kuahirisha mchezo kwa kuusogeza mbele ili hatua zingine zisifikiwe, maana mtu angeshuka daraja. Yangekuwa maamuzi magumu ambayo yangetuumiza,” alisema Mguto.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.