Mwigizaji wa filamu nchini, Hawa Hussein Ibrahim, almaarufu kama Carina au Caren, amefariki dunia leo, Aprili 15, 2025, akiwa nchini India.
Marehemu Carina alikuwa nchini humo kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya tatizo la tumbo lililokuwa likimsumbua kwa takriban miaka tisa.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Imelda Mtema, ambaye alikuwa mtu wake wa karibu.
Akizungumza na chombo cha habari cha Mwananchi, Bi. Mtema alisema amepokea simu kutoka India leo kuthibitisha taarifa hizo
“Ni kweli amefariki nimepigiwa simu leo na waliopo India, hata dakika 15 hazijapita, maana jana tu nimeongea naye,” alisema Imelda Mtema.
Inaelezwa kuwa mwigizaji huyo alikuwa amefanyiwa upasuaji mkubwa kutibu tatizo lake la tumbo, ambalo alikuwa akisumbuliwa nalo kwa muda mrefu na alikuwa amefanyiwa upasuaji mara 24 hapo awali. Alitarajiwa kurejea nchini leo baada ya kumaliza matibabu.
Carina aliondoka Tanzania kuelekea India Februari 24, 2025, baada ya kukamilika kwa taratibu za safari na kupatikana kwa gharama za matibabu kiasi cha Sh54 milioni, ambazo zilitokana na michango mbalimbali kutoka serikalini na taasisi nyingine.
Taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi zinatarajiwa kutolewa baadaye.
Mwigizaji Carina afariki dunia nchini India

Leave a Reply