Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa mwaka 2026 yameanza rasmi leo tarehe 19 Januari, 2026 katika Viwanja vya Usagara vilivyopo jijini Tanga. Maadhimisho hayo yameandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya fedha, ikiwemo matumizi sahihi ya huduma za kifedha, umuhimu wa kujiunga na mifumo rasmi ya fedha pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi kwa maendeleo endelevu.
Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Laswetula, ambaye ndio mgeni rasmi ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) baada ya kufika katika banda lao lililopo katika viwanja hivyo. Naibu Waziri Laswetula ameipongeza TADB kwa namna inavyofanya kazi katika kuchagiza mageuzi ya kilimo nchini kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara, namna ya kupata mikopo, umuhimu wa urasimishaji wa kilimo-biashara na mfuko wa dhamana ya mikopo kwa wakulima wadogo.
Aidha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu ya ufahamu kuhusu huduma zake huku ikieleza mafanikio yaliyofikiwa ikiwemo kuwafikia vijana zaidi ya 219 ndani ya mkoa wa Tanga katika mradi wa ‘wavuvi/boats’ kati ya hao wanawake ni 85 na wanaume 134.
Pamoja na hayo, TADB imefikia zaidi ya wafugaji 5,000 kwenye sekta ya maziwa tu, hii ni pamoja na vyama vya ushirika vya wafugaji na watu binafsi, huku kwa upande wa chai zaidi ya wakulima 600 wamefikiwa na wakulima wa Mpunga pia zaidi ya 200.
















Leave a Reply