Qatar kushirikiana na mamlaka za maji nchini kuimarisha mifumo ya usafi wa Mazingira

Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Dodoma (DUWASA) na Mtwara (MTUWASA) ikishirikiana na Ubalozi wa Tanzania Nchini Qatar, zimeahidiwa mashirikiano ya pamoja katika Sekta ya Usafi wa Mazingira hususani katika nyanja ya udhibiti na uondoshaji wa Majitaka katika Majiji na Manispaa za Mikoa.

Katika mazungumzo na ujumbe ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), Mhandisi Rejea Samweli ambaye aliishukuru Qatar kwa kuonyesha nia katika usimamizi wa Mifumo ya Usafi wa Mazingira katika Mamlaka za Maji Nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Majitaka wa Taasisi ya (ASHGAL) kutoka Qatar, AbdulAziz Ahmad, alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Nchini Qatar zimekuwa na mashirikiano mazuri ya muda mrefu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kiuchumi kwa manufaa ya Nchi zao.

“Tunatambua misingi imara ya muda mrefu iliyowekwa na Watangulizi wetu katika kuimarisha mahusiano. Sisi kama Taasisi ya mifumo ya Majitaka tunaahidi kusaidiana na Tanzania katika upande wa wataalam wa technolojia ya mifumo” alisisitiza

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Habibu Awesi Mohammed, aliwashukuru Mamlaka za Maji DAWASA, DUWASA na MTUWASA na NEMC kwa kuonesha nia ya kujifunza Nchini Qatar juu ya usimamizi wa mifumo ya Usafi kwa manufaa ya Watanzania.

Ziara hiyo pia imewashiriki Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).