Rais wa Marekani, Donald Trump, ametia saini tangazo la kupiga marufuku raia wa mataifa 12 kuingia nchini Marekani, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zikiwanukuu maafisa wa utawala wake. Tangazo hilo linazuia kabisa na kuwawekea mipaka raia wa mataifa hayo kuingia Marekani.
Mataifa yaliyoathirika na marufuku kamili ni pamoja na Afghanistan, Myanmar, Chad, Kongo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen, kulingana na kituo cha utangazaji cha CBS. Aidha, raia wa mataifa mengine saba – Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela – watawekewa zuio la kiwango fulani.
Hatua hii inarejelea marufuku kama ile aliyoipiga wakati wa muhula wake wa kwanza, ambapo aliwazuia wasafiri kutoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia Marekani. Marufuku hiyo ya awali ilipingwa kisheria na hatimaye ilibatilishwa na Rais Joe Biden mnamo mwaka 2021, akisema ilitia doa taifa hilo.
Leave a Reply