Salah asaini mkataba mpya kusalia Anfield hadi 2027

Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah, amesaini rasmi mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamuweka Anfield hadi Juni 2027. 

Hatua hiyo inamaliza uvumi uliodumu kwa miezi kadhaa kuhusu mustakabali wa Salah, hasa baada ya kuvutiwa na ofa kutoka kwa klabu za Ligi Kuu ya Saudi Arabia.  

Mkataba huo mpya unaripotiwa kuwa na thamani ya pauni milioni 41.6 kwa miaka miwili, sawa na mshahara wa takriban pauni 400,000 kwa wiki pamoja na bonasi. 

Hii inamfanya Salah kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika Ligi Kuu ya England. 

Awali, kulikuwa na taarifa kuwa Salah alikuwa hajapokea ofa yoyote ya kuongeza mkataba wake, lakini sasa ameamua kubaki Liverpool, akisisitiza kuwa anafurahia maisha na soka ndani ya klabu hiyo.

Tangu ajiunge na Liverpool mwaka 2017 kutoka AS Roma, Salah amekuwa mchezaji muhimu kwa mafanikio ya klabu hiyo. Amefunga jumla ya mabao 243 na kutoa pasi za mabao 111 katika mechi 394. 

Kwa msimu huu pekee, amefunga mabao 32 na kutoa pasi 22 katika mechi 45, akiongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu akiwa na mabao 27 katika Ligi Kuu.  

Kusaini kwa Salah ni habari njema kwa kocha mpya wa Liverpool Arne Slot, kwani Liverpool inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 11 huku zikiwa zimesalia mechi saba. 

Uwepo wa Salah unaongeza matumaini ya kutwaa taji la 20 la ligi.

Kwa ujumla, uamuzi wa Salah kubaki Liverpool unaonyesha dhamira yake ya kuendelea kuandika historia na kufanikisha ndoto zake za soka akiwa Anfield.