Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa ameeleza kuwa Serikali iko tayari kushughulikia na kutatua changamoto mbalimbali zinazoleta mkwamo kwa Shirika la Posta Tanzania (TPC) katika kutimiza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.
Ameyaeleza hayo leo tarehe Januari 10, 2025 wakati Uzinduzi na Ufunguzi wa Mkutano wa 31 wa Baraza kuu la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, katika ukumbi wa mikutano wa NSSF, jijini Dar Es Salaam
Akiongea wakati wa ufunguzi huo, Waziri Silaa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta kuongeza ubunifu, weledi sambamba na kupanga mikakati bora katika utoaji wa huduma za Shirika ili kuongeza pato la Shirika na hatimaye gawio kwa mwenye hisa.
Aidha Mhe. Silaa ameongeza kuwa kupitia mkutano huo wa Baraza, wafanyakazi wawe huru katika kuchangia hoja na kuwa wawazi katika kutoa mapendekezo yenye tija ili maazimio yatakayofikiwa yawe chanya kwa maslahi mapana kwa Serikali, Shirika na wananchi kwa jumla.
Kwa upande wake Bw. Mulembwa Munaku kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amelipongeza Shirika la Posta kwa kuwa na vikao hivi kila mwaka ambavyo vinasaidia kujadili na kutathmini mwenendo wa Shirika, na kuwawezesha wafanyakazi wote kujua majukumu yao kwa kushirikiana.
Naye, Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kuongeza kuwa kwa kushirikina na wafanyakazi watazifanyia kazi changamoto zilizopo ndani ya Shirika ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kulingana na mahitaji ya sasa ya wananchi.
Leave a Reply