Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewaasa watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika ujenzi wa majengo ya kisasa na vifaa tiba.
Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha hayo leo (10.01.2025) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika hospitali hiyo kufanya ukaguzi wa vifaa tiba na utolewaji wa huduma za afya ambapo serikali imewekeza ujenzi wa Shilingi Bilioni 5.6 pamoja na Shilingi Milioni 500 ya vifaa mbalimbali vya tiba vimenunuliwa ili kuongeza huduma za afya.
Amewaasa watumishi hao kuzingatia maadili na utendaji uliotukuka katika majukumu yao ili wagonjwa wapate huduma nzuri kwa kuwa mtaji mkubwa wa binadamu ni afya ili aweze kutekeleza majukumu yake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji anafanya ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Tanga ambapo leo hii yupo Wilayani Handeni katika siku ya nne ya ziara hiyo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi miradi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika Mkoa wa Tanga, kupitia kauli mbiu ya “Waone na Wasikie.”
Leave a Reply