Simba Mbele ya Kibarua Kigumu Kufuzu Nusu Fainali ya CAF Confederation Cup

simba vs al masry

Simba Mbele ya Kibarua Kigumu Kufuzu Nusu Fainali ya CAF Confederation Cup. Simba SC wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Masry kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali, uliochezwa Aprili 2, 2025, huko Ismailia, Misri.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa New Suez ulianza kwa kasi, huku wenyeji wakitumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kushambulia kwa nguvu tangu dakika za mwanzo. Mashabiki wa Al Masry walilipuka kwa furaha dakika ya 16 baada ya Abderrahim Deghmoum kufunga bao la kwanza akimalizia pasi murua kutoka kwa Youssef El Gohary.

Baada ya bao hilo, Al Masry walilegeza kasi yao, hali iliyowawezesha Simba kupata udhibiti wa mpira na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Hata hivyo, ukosefu wa umakini kwenye safu ya ushambuliaji pamoja na uimara wa kipa wa Al Masry, Mahmoud Gad, uliwafanya Wekundu wa Msimbazi kushindwa kusawazisha hadi mapumziko, wakiwa nyuma kwa bao moja.

Simba Walipambana Lakini Ngoma Ilikuwa Nzito

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kucheza kwa kasi wakitafuta bao la kusawazisha. Elie Mpanzu aliisumbua safu ya ulinzi ya Al Masry mara kadhaa, lakini tatizo la umaliziaji liliendelea kuwagharimu.

Eli Mpanzu ndani ya mchezo

Fursa nzuri zaidi kwa Simba ilikuja dakika ya 85 baada ya beki wa kulia, Shomari Kapombe, kupokea pasi safi kutoka kwa Steven Mukwala. Hata hivyo, shuti lake halikuzaa matunda baada ya kipa Gad kuokoa kwa umahiri mkubwa.

Dakika moja baadaye, Gad tena alikuwa mwiba kwa Simba baada ya kupangua kombora la Kapombe lililotoka nje ya eneo la hatari.

Simba walionekana kuwa na matumaini ya kutoka na kipigo cha bao moja tu, lakini matumaini hayo yaliishia dakika ya 89 baada ya mshambuliaji wa Al Masry, John Ebuka, kufunga bao la pili. Bao hilo lilihitaji uhakiki wa VAR kabla ya kuthibitishwa na mwamuzi kutoka Mali, Boubou Traore.

Takwimu za Mchezo

Licha ya kufungwa, takwimu zilionyesha kuwa Simba walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi. Walipiga mashuti 18 dhidi ya 7 ya Al Masry na walimiliki mpira kwa asilimia 51, huku wenyeji wakimiliki asilimia 49. Hata hivyo, kushindwa kutumia nafasi walizopata kulikuwa pigo kubwa kwao.

Kibarua Kizito Mkapa

Simba sasa wanakabiliwa na mtihani mgumu kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Aprili 9, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Ili kufuzu hatua ya nusu fainali, wanahitaji ushindi wa angalau mabao 3-0.

Kwa faida ya kucheza nyumbani na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao, Simba wanahitaji kucheza kwa umakini mkubwa, kutumia kila nafasi wanayopata, na kuhakikisha ulinzi wao unadhibiti mashambulizi ya Al Masry.

Je, wataweza kupindua matokeo na kusonga mbele, au ndoto yao ya kutinga nusu fainali itaishia hapa? Majibu yatapatikana baada ya dakika 90 za mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.

Alichokisema Kocha wa Simba Fadlu David baada ya matokeo