Simba SC Kuumana na Stellenbosch FC Katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC)

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Zamalek SC kutoka Misri, wametupwa nje ya michuano hiyo baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini. Matokeo haya yameandika historia mpya kwa timu ya Stellenbosch, ambayo sasa imejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza kabisa.

Kwa upande mwingine, Simba SC ya Tanzania, ambayo ilitinga nusu fainali baada ya kuibwaga Modern Future ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2, sasa itakutana uso kwa uso na Stellenbosch katika mechi mbili za kuamua nani ataingia fainali ya CAF Confederation Cup msimu huu wa 2024/2025.

Ratiba Rasmi ya Mechi za Nusu Fainali:

Simba SC vs Stellenbosch FC
Tarehe: Jumapili, Aprili 20, 2025
Uwanja: Benjamin Mkapa Stadium, Dar es Salaam

Stellenbosch FC vs Simba SC
Tarehe: Jumapili, Aprili 27, 2025
Uwanja: Danie Craven Stadium, Stellenbosch, Afrika Kusini


Simba SC wataanzia nyumbani katika dimba la Benjamin Mkapa, wakihitaji kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani na sapoti ya mashabiki ili kujipatia matokeo mazuri kabla ya kurejea Afrika Kusini kwa mechi ya marudiano.

Kwa kuzingatia ubora wa timu zote mbili, hii inatarajiwa kuwa mchuano wa kusisimua na wenye ushindani mkali. Stellenbosch imeonekana kuwa tishio kwa timu kubwa msimu huu, lakini Simba SC wana uzoefu mkubwa katika mashindano ya Afrika na wataingia dimbani wakiwa na malengo makubwa ya kufika fainali na hatimaye kutwaa taji.

Je, Mnyama ataweza kuvuka kihunzi hiki kigumu? Mashabiki wa Simba na wapenda soka kwa ujumla wanasubiri kwa hamu kuona kama wekundu wa Msimbazi wataendeleza moto wao na kuweka historia mpya katika soka la Afrika.