Simba SC Yatinga Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho kwa Ushindi wa 2-1
Simba SC imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Big Man FC ya Tanga. Mchezo huo ulipigwa leo katika Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Katika mtanange huo wa michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB, Simba SC ilianza vyema kwa kutangulia kupata bao kupitia winga wake kutoka Zambia, Joshua Mutale, aliyefunga dakika ya 16.

Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Cameroon, Christian Leonel Ateba Mbida, aliongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 31.

Hata hivyo, Big Man FC walipambana na kufanikiwa kupata bao pekee kupitia kwa Joseph Henock sekunde chache kabla ya mapumziko dakika ya 45. Licha ya juhudi zao katika kipindi cha pili, hawakuweza kusawazisha, na hivyo Simba SC wakaondoka na ushindi muhimu uliowapa tiketi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Simba SC sasa inasubiri droo ya hatua inayofuata ili kujua wapinzani wake katika harakati za kutwaa taji hilo.
Leave a Reply