Sudan ni wabishi asikuambie mtu. Hadi sasa wameshakata tiketi ya kushiriki mashindano ya Michuano ya Mataifa Afrika (AFCON 2025) huku wakiwatimulia vumbi tu wapinzani wao wa karibu ambao ni Ghana.
Sudan hii pia inaongoza msimamo wa kundi lake kufuzu Kombe la Dunia wakifuatiwa na vigogo Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ikumbukwe kuwa hili ni taifa ambalo limepitia hekaheka za vita, ikishuhudiwa Wasudan wakiuana wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka miwili.
Vita hizo ndio sababu kuu iliyopelekea Sudan kucheza mechi zake za Kimataifa katika viwanja tofauti mbali na nyumbani.
Sio tu kikosi cha Taifa hilo kilichokumbwa na changamoto hiyo kwani hata klabu kubwa zake kubwa za Al-Hilal na Al-Merrikh msimu huu zinasakata kandanda huko nchini Mauritania.
Si haba, timu ya taifa ya Sudan imekuwa ndio tulizo safi la nafsi za Wasudan wote ambao pengine bado wana kumbukumbu mbaya ya kupoteza ndugu, jamaa na marafiki waliokatishwa maisha kutokana na vita.
Na baada ya kipindi kirefu sana Wasudan sasa wanaweza kuota ndoto nzuri ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi hiyo.
Mchezo wa mpira wa miguu hutumika kuangaza nyakati za giza nene na kwa hiki kinachotokea upande wa Sudan ni mfano halisi na unaopendeza.
Shukrani za Wasudan zinaelekezwa moja kwa moja hadi kwa nguli wa Ghana, Kwesi Appiah, ambaye ndiye kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Sudan tangu 2023 akiwaongoza kupata matokeo bora uwanjani na kuwapaisha kwenye anga la Soka Afrika kama lilivyo jina lao la utani la “MWEWE WA JEDIANE”
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.