NA KELVIN LYAMUYA
KUNA kipindi jamii ya soka iliweka imani kubwa kwa Joao Felix kiasi cha kuufananisha uwezo wake na Ricardo Kaka.
Leo hii nadhibitisha kwamba kitu pekee kinachowafananisha Joao Felix na Ricardo Kaka ni muonekano wa sura tu.
Hayo ya kufanana sura wala sio muhimu sana, unataka kujua nini hasa kilichonisukuma nitake kuwazungumzia Felix, Thomas Muller, Paulo Dybala na Antoine Griezmann? Twenzetu….
Katikati ya 2009 na 2010, chipukizi Muller akiwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia pale Afrika Kusini, huku kinda mwingine, Griezmann akifunga mabao 5 katika mechi nne za pre-season pale Sociedad na kukabidhiwa jukumu la kucheza winga ya kushoto bila kupitia timu ya akiba (reserve team) ndipo ulimwengu wa soka ulipowakaribisha mafundi wawili kwa shangwe la kutosha.
Muller na Griezmann waliposimika himaya zao, kiwanda cha soka kikatuletea Dybala ambaye dili lake la kutoka Palermo kwenda Juventus lilitikisa Italia kiasi cha bosi wa Juve enzi hizo, Maurizio Zamparini, kumtabiria makubwa zaidi ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo!

Dybala akazichana sana nyavu za wapinzani hadi kuvunja rekodi za mkongwe Alessandro del Piero, hicho tu kilitosha kuwaaminisha wadau kwamba jamaa ni moto wa kuotea mbali. Akayabeba makombe ya kutosha ya Scudetto. Leo hii yuko AS Roma. Tofauti na matarajio ya wengi kwamba angeishia Real Madrid, Barcelona au Manchester United.
Uzuri wa maisha ya wanasoka huwa yanaingiliana katika nyakati zinazofuatana kama vifaranga. Mtiririki wa historia hii unamalizikia kwa Joao Felix wa 2018 akiwa Benfica, kipindi ambacho Dybala ni almasi inayong’aa pale Juventus.
Mwanzoni mwa makala haya nilieleza mwanzo wa Felix na matarajio ya watu juu yake lakini kutoka Benfica kwenda Atletico Madrid hadi kuwa mchezaji wa kutolewa kwa mkopo Chelsea (x2), Barcelona na sasa AC Milan, masikitiko lazima yawe makubwa, labda ataimarika tena huko Italia ambako soka la huko liko juu sana kwa sasa.
Wachezaji hawa wanne, wanacheza katika nafasi sawa. Kiungo mshambuliaji au mshambuliaji msaidizi au hata kiungo huru namba 8 lakini walichokosa Dybala na Felix na kikawapa heshima Muller na Griezmann ni uwezo wa kubadilika kulingana na nafasi zaidi ya moja wanazocheza (adaptability).
Kucheza kwao katika nafasi zinazofanana kumewaweka katika kundi moja lakini katika misingi halisi ya soka, mipaka ya ubora wao imewatenganisha katika makundi mawili; ‘Mediapunta’ neno la Kihispania lenye maana ya ‘False 9’ au lugha nyepesi kiungo mshambuliaji (Dybala, Felix).

Halafu kundi la pili ndio hili la Muller na Griezmann ambao binafsi nawaona ni washambuliaji wasaidizi wanaozalisha vitu vingi sana kwenye eneo la mwisho na pia wamebarikiwa ufundi (technically gifted).
Utofauti wa makundi hayo mawili unabebwa na hoja ya kwamba; kocha mwenye hadhi na uwezo mkubwa duniani angediriki hata kuua ili aipate saini ya Griezmann au Muller na sio Dybala wala Felix.
Klabu yenye watu makini katika uongozi lazima ijitutumue ili kumsajili mchezaji mwenye quality ya Griezmann au Muller ambao kuanzia klabu na kimataifa kote huko wametisha. Kuanzia Muller wa 2010 hadi Griezmann wa Euro 2016.
Lakini ni nani ambaye yuko radhi kujitoa ufahamu kwa Dybala na Felix? Hakuna.
Kwani si ndio Griezmann huyu huyu ambaye hakudumu Barcelona lakini bado alizalisha jumla ya magoli/asisti 52, huku akicheza nje ya nafasi aliyoizoea sambamba na Messi? Ndio nilichosema sasa, ADAPTABILITY.
Hicho ndio kilimchemsha Dybala. Tena alichemka hadi akajitokeza hadharani kwamba suala la yeye kucheza pamoja na Messi timu ya Taifa Argentina ni mtihani uliomshinda.
Nitakuwa wa kwanza kukiri kwamba Griezmann na Müller wana uwezo hata wa kutumika kama viungo wawili wa kati (double pivot) na wakacheza vizuri tu. Na nitakuwa wa mwisho kuamini Dybala na João Félix wana uwezo wa kufanya makubwa katika timu isiyokidhi mahitaji yao kimbinu hata kama wakitumika kama namba 9!
Muller ni shujaa wa Bayern Munich na klabu yoyote kubwa duniani ambayo ilijaribu kumsajili na ikamkosa. Vivyo hivyo pia kwa Griezmann. Lakini hawa wengine ni hadi wapate timu yenye mazingira bora kwao au kocha mwenye mbinu au mipango fulani.

Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.