Wasira aeleza sababu za CCM Kuhitajika milele

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira ameeleza mambo mbalimbali yanayoifanya CCM kuwa idumu.

Mojawapo ya sababu hizo ni wajibu wake wa majukumu endelevu ya kuwatumikia Watanzania.

Amesema kutokana na umuhimu wa majukumu hayo kwa ustawi wa nchi na maisha ya Watanzania CCM itakuwepo wakati wote.

Wasira ameyasema hayo leo Juni, 16, 2025 alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ambako ameanza ziara ya siku tatu ya kukagua uhai wa Chama, kuzungumza na wana CCM na makundi mbalimbali yakiwemo ya viongozi wa dini, wakulima na wafugaji.

“CCM ni Chama kikubwa na chenye historia, watu wengi wanadhani CCM ilianza miaka 48 iliyopita, Chama hiki kimerithi mikoba ya vyama vya TANU na Afro Shiraz Party. TANU ina miaka 75 na Afro Shirazi Part y miaka 67.

“CCM ni Chama kipya ambacho kimeundwa na vyama vya zamani. Kimekabidhiwa majukumu ya kudumu, hivyo tukisema kidumu Chama Cha Mapinduzi hatuna utani. Tunazungumza kidumu Chama kwa sababu kina majukumu ya kudumu ambayo tumekabidhiwa tangu kuanzishwa kwake,” amesema.

“Hivyo umoja ni kazi ya CCM tuliyokabidhiwa na sasa umoja na amani ya nchi yetu imekuwa tunu ya Watanzania wote. Kwa hiyo ukianzisha jambo lako likapolewa na likakubaliwa na watu wote linakuwa lako lakini pia linakuwa la wote,” alisema.

Wasira amesisitiza kuwa kazi ya CCM ni kuendelea kujenga umoja wa watu wote na kufafanua kuwa, Tanzania iko tofauti na mataifa mengine ya Afrika kwa kuwa haina ukabila wala udini.