Yanga Yaambiwa Hakuna Alama 3 Inaweza Kushushwa Daraja Kwa Kutofata Kanuni (47:18)

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB) imejibu barua ya klabu ya Yanga inayohitaji kupewa alama 3 pamoja na mabao 3 kwa mchezo ulioahirishwa tarehe 8 Machi, 2025. Ingawa taarifa hii haijathibitishwa rasmi, vyanzo vya habari vinasema kuwa barua ya Bodi iliyotolewa tarehe 16 Machi, 2025, yenye kumbukumbu Na TPLB/CEO/2024/625 inadai kuwa mechi hiyo iliahirishwa kwa kufuata kanuni na si kwa sababu ya Simba SC kugomea kama ilivyosema Yanga.

Taarifa hiyo inadai kuwa mchezo uliahirishwa rasmi saa 8 mchana, na baada ya hapo, hakukuwa na taratibu zozote za mchezo ambazo ziliendelea, isipokuwa shughuli za usalama pekee. Maafisa wa mchezo waliondoka uwanjani, na hakukuwa na hatua yoyote za kifasihi zilizofuatwa ili kumpatia alama 3 na mabao 3 timu yoyote, kama inavyosema kanuni ya 17.

Vyanzo hivi pia vinadai kuwa Bodi ilieleza kuwa klabu ya Yanga inapaswa kuelewa kwamba kanuni za Ligi Kuu, namba 17:45, haziwezi kudai kwamba klabu mgeni inapaswa kuwasiliana na wadau wengine kwa ajili ya mazoezi kabla ya mchezo, kama inavyodaiwa na Yanga.

Aidha, Bodi ilibainisha kuwa Kamati ya Uendeshaji ya Ligi ilikusanya taarifa kuhusu mgogoro wa tarehe 7 Machi, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Simba walitaka kufanya mazoezi na kutokea kwa matukio yaliyoleta taharuki. Kamati iliona umuhimu wa kuahirisha mechi ili kuepuka changamoto za kiusalama, na kujipa muda wa kufanya uchunguzi zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya uchunguzi vya kitaifa.

Bodi ilieleza kuwa, licha ya kuahirishwa kwa mechi, Yanga walikiuka kanuni ya 47:18 kwa kupeleka timu uwanjani, hali inayoweza kupelekea adhabu ya kushushwa daraja au hatua zingine za kinidhamu.