Young Africans Yasisitiza Kutocheza Kariakoo Derby Licha ya Mazungumzo na Waziri
Klabu ya Young Africans imesisitiza msimamo wake wa kutoshiriki mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Simba SC, licha ya mazungumzo yaliyofanyika kati ya viongozi wa klabu hiyo na Waziri mwenye dhamana ya michezo. Mchezo huo, ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 8, umeendelea kuzua mjadala mkubwa kutokana na msimamo wa Yanga wa kutoshiriki.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alieleza kuwa licha ya kikao chao na Waziri siku ya jana, bado klabu imeamua kusimamia msimamo wake. “Tumekaa na Waziri tukazungumza, lakini uamuzi wa klabu bado uko pale pale. Hatutashiriki mechi hiyo kwa sababu zetu wenyewe, ambazo tayari tumezieleza,” alisema Ali Kamwe.
Kikao hicho kilifanyika kwa lengo la kutafuta suluhu kuhusu mgogoro huo, huku wadau wa soka wakitarajia kuwa lingesaidia kufanikisha derby hiyo kubwa inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini. Hata hivyo, Young Africans imeendelea kushikilia msimamo wake, hali inayoacha sintofahamu kuhusu hatma ya mchezo huo.
Kauli hiyo ya Yanga ilitolewa mara baada ya klabu hiyo kutia saini makubaliano na Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, ambapo imekubali kushiriki katika kuitangaza Zanzibar kupitia kampeni ya “Visit Zanzibar.” Makubaliano haya yanatajwa kuwa hatua muhimu kwa klabu hiyo, inayotumia ushawishi wake kuvutia watalii na kuinua utalii wa Zanzibar kupitia mashabiki wa soka.
Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki wa soka yanaelekezwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mamlaka husika ili kuona hatua zitakazochukuliwa kuhusu mustakabali wa mechi hiyo, huku Simba SC ikiendelea na maandalizi yake kwa mchezo huo kama kawaida.
Young Africans Yasimamia Uamuzi wa Kutocheza Kariakoo Derby

Leave a Reply