FIFA yaifungia uanachama FECOFOOT ya Congo

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelisimisha uanachama Shirikisho la Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT) mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Kwa mujibu wa barua ya FIFA kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), uamuzi huo wa kuisimamisha FECOFOOT umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 16 ya Katiba ya FIFA.

Taarifa ya TFF imeeleza kuwa Uamuzi huo umefanywa Juzi, Februari 6, 2025 na kuanzia hapo FECOFOOT imepoteza haki zote za uanachama kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 13 ya Katiba ya FIFA.

Hivyo, FECOFOOT pamoja na klabu zake hazitashiriki katika mashindano yoyote ya kimataifa mpaka hapo adhabu hiyo itakapoondolewa.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa FECOFOOT, wanachama wake na maofisa wake hawatanufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo kutoka FIFA au Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika kipindi hiki ambapo wanatumikia adhabu hiyo.

Pia wanachama wa FIFA pamoja wanachama wao wanakumbushwa kutokuwa na uhusiano wowote wa kimichezo na FECOFOOT au wanachama wake katika kipindi hiki ambapo FECOFOOT imesimamishwa.