Yanga Princess yafuta ‘unbeaten’ ya Simba Queens WPL2025

Kikosi cha Timu ya Wanawake ya Yanga, (Yanga Princess) kimeiadhibu timu ya wanawake ya Simba, Simba Queens kwa kichapo cha bao 1-0 lililofungwa na Jeannnine Mukandayisenga katika Uwanja wa KMC Complex, Jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili kwa Yanga Princess kushinda mbele ya Simba Queens kwenye michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake baada ya ule ushindi wa Aprili 24, 2022 goli lilifungwa na Nyota wa Al Nassr, Clara Luvanga chini ya Kocha, Edna Lema.

Simba Queens wamecheza michezo 12 ya Ligi Kuu ya wanawake msimu wa 2024/25 bila kupoteza mchezo wowote huku wakishika nafasi ya kwanza Kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 34 kabla ya Yanga Princess kutibua mtiririko huo katika mchezo wa 13.

Ikumbukwa pia Katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Ligi Kuu ya Wanawake uliofanyika Oktoba 2, 2024, Yanga Princess ilifanikiwa kuiondoa Simba Queens kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.

Yanga Princess inashika nafasi ya tatu katika mchezo huo, wamecheza michezo 13 na kujikusanyia alama 27 na katika mzunguko wa pili wamecheza michezo minne ya Ligi bila kupoteza mchezo wowote.