Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Taifa Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati afariki dunia

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wafula Chebukati, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 63. Kaka yake, Daniel Chebukati, amethibitisha kifo hicho, akieleza kuwa Wafula alikuwa amelazwa hospitalini kwa takriban wiki moja akipokea matibabu, ingawa ugonjwa uliosababisha kifo chake haujawekwa wazi.

Wafula Chebukati alihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita, kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2023. Katika uongozi wake, alisimamia chaguzi kuu mbili nchini Kenya: Uchaguzi Mkuu wa 2017 na Uchaguzi Mkuu wa 2022. Pia, aliongoza katika Uchaguzi wa Marudio wa Rais uliofanyika Oktoba 2017. Baada ya kustaafu, alikabidhi rasmi majukumu yake mnamo Januari 17, 2023.

Rais wa Kenya, William Ruto, kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), alielezea huzuni yake kufuatia kifo cha Chebukati, akisema: “Kenya imepoteza mtu muhimu. Salamu zetu za pole kwa familia, ndugu na marafiki wa Wafula Chebukati.”

Kabla ya kujiunga na IEBC, Chebukati alikuwa wakili mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 37, akimiliki na kuendesha kampuni yake binafsi ya sheria kwa zaidi ya miaka 20. Alikuwa na utaalamu katika sheria za biashara, sheria za makampuni, usimamizi wa makampuni, na utatuzi wa migogoro. Pia, aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na aligombea kiti cha ubunge cha Jimbo la Saboti mwaka 2007, ambapo alishika nafasi ya pili.

Kwa mchango wake katika huduma ya umma, Chebukati alitunukiwa nishani ya Elder of the Order of the Golden Heart (EGH), ambayo ni tuzo ya pili kwa hadhi kubwa inayotolewa na serikali ya Kenya.

Kifo cha Chebukati ni pigo kubwa kwa taifa la Kenya, hasa ikizingatiwa mchango wake katika kusimamia chaguzi muhimu na kuhakikisha demokrasia inaendelea kustawi nchini humo.