Morocco Yaizamisha Taifa Stars 2-0, Nafasi ya Tanzania Kufuzu Kombe la Dunia Yapungua

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepata pigo baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Morocco kwa mabao 2-0 katika mchuano wa kufuzu Kombe la Dunia 2026. Mechi hiyo ilichezwa tarehe 26 Machi 2025, ikiwa ni sehemu ya hatua za makundi za kufuzu kwa bara la Afrika.


Mchezo Ulivyokuwa
Mchezo ulianza kwa kasi, huku Taifa Stars ikijaribu kujilinda dhidi ya mashambulizi makali ya Morocco. Hata hivyo, juhudi zao hazikufua dafu kwani dakika ya 51, beki Nayef Aguerd aliifungia Morocco bao la kwanza kwa shuti fupi kufuatia mpira wa kona.

Dakika saba baadaye, Morocco walipata penalti baada ya Ibrahim Hamad kushika mpira ndani ya eneo la hatari. Brahim Díaz alitumia vyema nafasi hiyo na kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 58, na kufanikisha ushindi wa 2-0 kwa Morocco.

Mchezaji Bora wa Tanzania
Katika mchezo huu, Kibu Dennis alionekana kuwa mchezaji mwenye kiwango bora zaidi upande wa Tanzania, akipata rating ya 7.0. Hii ilimfanya kuwa mchezaji pekee wa Taifa Stars aliyefikia kiwango hicho, huku wenzake kama Yakoub Suleiman (6.8) na Feisal Salum (6.7) wakishindwa kufikia viwango vya juu zaidi.

Kibu Dennis ndani ya mchezo.

Kwa upande wa Morocco, Noussair Mazraoui alikuwa mchezaji bora wa mchezo, akipata rating ya 8.0. Beki huyo wa Manchester United alionyesha kiwango cha juu kwa kuchangia katika ulinzi imara wa Morocco na kusaidia timu yake kushinda kwa mabao 2-0.

Noussair Mazraoui

Wachezaji wengine wa Morocco waliocheza kwa kiwango kizuri ni Nayef Aguerd (7.9), aliyefunga bao la kwanza la mchezo, na Jawad El Yamiq (7.9), ambaye alifanya kazi nzuri katika safu ya ulinzi na kushambulia kwa mipira ya kona na krosi.

Kwa ujumla, Morocco walitawala mchezo kwa kiwango kikubwa, wakitumia vyema nafasi zao na kuonyesha ubora wa kikosi chao.

Nafasi ya Taifa Stars Kufuzu
Baada ya matokeo haya, nafasi ya Tanzania kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 inazidi kuwa ngumu. Taifa Stars italazimika kushinda mechi zake zijazo na kutegemea matokeo ya timu nyingine ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu.

Kwa sasa, Morocco inaendelea kuongoza kundi lake kwa pointi 15 baada ya ushindi huo, huku Tanzania ikijipanga kurekebisha makosa yake kwa mechi zijazo.

Taifa Stars sasa inapaswa kujipanga upya kwaajili ya mechi zijazo ili kuhakikisha inapata matokeo mazuri na kuweka hai matumaini ya kufuzu Kombe la Dunia 2026

Msimamo wa kundi baada ya mechi ya leo